Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir amelivunja bunge lake na kuunda serikali ya umoja, katika harakati za kupiga jeki makubaliano ya amani yanayolenga kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vya takriban miaka miwili.
Mpango huo unaowashirikisha waliokuwa waasi katika serikali ulitangazwa Alhamisi katika runinga ya taifa.
Thuluthi moja ya mawaziri wa bunge hilo jipya ni wanachama wa chama cha SPLM-IO kilichobuniwa na aliyekuwa kiongozi wa waasi Riek Machar,ambaye alirudi mjini Juba mapema wiki hii ili kuapishwa kuwa makamu wa kwanza wa rais.
Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa aliunga mkono hatua hiyo kama ya kihistoria katika makubaliano hayo ya amani.
Makumi ya maelfu wameuawa na watu milioni 2 wakiwachwa bila makao katika mgogoro huo wa Sudan Kusini ambayo ilipata uhuru wake mwaka 2011.
Mwandani wa rais Salva Kiir Kuol Manyang atasalia kuwa waziri wa Ulinzi na David Deng Athorbei akiwa waziri wa fedha ambao watajaribu kuimarisha uchumi ulioathiriwa na vita vya zaidi ya miaka miwili.
Wizara muhimu ya mafuta ilipewa Dak Duop Bichok.
Wizara ya kigeni imechukuliwa na Deng Alor wadhfa alioshikilia chini ya serikali moja ya Sudan kabla ya Sudan Kusini kupata uhuru wake mwaka 2011.
Alor alikuwa mwanachama wa kundi linalojiita ''wafungwa wa zamani'',viongozi wenye ushawishi waliokamatwa wakati vita vilipoanza,lakini baadaye wakaachiliwa baada ya shinikizo kali.
Kiongozi wa upinzani na mkosoaji mkubwa Lam Akol atakuwa waziri wa kilimo na usalama wa chakula,ikiwa ni wizara muhimu ambapo watu milioni tano wanahitaji msaada,huku maeneo mengine yakikabiliwa na ukame.