Baada ya siri ya ugonjwa uliosababisha kifo cha aliyekuwa Waziri
wa fedha, Dk William Mgimwa ikidumu kwa siku kadhaa, baadaye Serikali ilisema
kilichosababisha kifo chake ni ugonjwa wa figo.
Dk Mgimwa alifariki Januari Mosi, mwaka huu katika Hospitali ya
Kloof Medi Clinic, Pretoria nchini Afrika Kusini alikokuwa amelazwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dk Servacius Likwelile uliutaja
ugonjwa huo mbele ya waombolezaji waliofika kuuaga mwili wake kwenye Viwanja
vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Likwelile alisema: “Marehemu Mgimwa alikwenda Hospitali ya Kloof
Medi Clinic, Afrika Kusini Novemba 3, mwaka 2013 kwa ajili ya uchunguzi wa
kawaida wa afya yake. Baada ya uchunguzi, madaktari walimshauri alazwe kwa
uangalizi zaidi na matibabu na kwamba aliendelea na matibabu ya figo hadi kifo
chake.”
Kwa nini figo hushindwa kufanya kazi?
Figo ni viungo vilivyomo ndani ya mwili vyenye kazi ya kuchuja
uchafu uliomo kwenye damu. Vinahusika pia na uratibu wa shinikizo la damu,
madini yenye umeme ndani ya damu na uzalishaji wa chembe nyekundu za damu.
Kati ya sababu nyingi za figo kushindwa kufanya kazi ni
shinikizo la juu la damu na ugonjwa wa kisukari. Kwa takwimu inaonyesha kuwa
zaidi ya nusu ya watu wazima wenye matatizo ya figo husababishwa na magonjwa
hayo.
Kwa kisukari; kama haujatibiwa ipasavyo, sukari itajijenga ndani
ya damu na ikiwa nyingi huharibu seli hivyo hupunguza uwezo wa figo kuchuja
uchafu.
Kuna aina mbili za kisukari, kwanza kisukari ambacho mwili
unashindwa kuzalisha tezi inayomeng’enya sukari kwenye damu (insulin). Kisukari
cha pili ni pale mwili unaposhindwa kutumia vizuri insulin inayozalishwa.
Kwa tatizo la shinikizo la juu la damu; ni pale kunapokuwa na
shinikizo kubwa la damu kuliko ukubwa wa mishipa yake. Kama shinikizo hilo
litaongezeka litasabisha ugonjwa wa moyo, mshtuko na ugonjwa sugu wa figo.
Sababu nyingine ni kuharibika kwa seli zinazohusika na uchujaji
wa uchafu hali inayosababisha kupungua kwa mkojo, kutokutolewa kwa protini
katika mkojo na kuvimba kwa mikono na miguu.
Nyingine ni magonjwa ya kurithi kama vile ‘Polycystic’ yaani
vivimbe kutokea ndani ya figo hivyo kushindwa kufanya kazi. Magonjwa kama
haya siyo ya kawaida lakini huanza wakati mtoto akiwa bado tumboni.
Dalili
Dalili za kushindwa kwa figo ni pamoja na kuongezeka kwa uchafu
ndani ya mwili ambao husababisha udhaifu, kuhema kwa shida, uchovu na
kuchanganyikiwa. Kushindikana kuondolewa kwa kemikali ya potasiamu katika
mirija ya damu husababisha mapigo ya moyo na kifo cha ghafla. Wakati mwingine
dalili zinaweza zisijitokeze hata kama tatizo lipo.
Uchunguzi wa magonjwa ya figo hufanywa kwa kupima kemikali ya
urea ya naitrojeni iliyomo kwenye damu na kuchunguza kiwango cha uchujaji
wa uchafu (glomerular filtration rate -GFR).
Kama matibabu yatakwenda vizuri figo inaweza kurudia katika hali
yake ya kawaida. Kujiepusha na shinikizo la damu na kujilinda na kisukari ni
njia bora za kujilinda na magonjwa sugu ya figo. Kwa kawaida utendaji wa
figo hupungua kwa jinsi umri unavyoongezeka.
Figo ikishindikana kabisa kutibika, kinachofanywa ni kuchuja
uchafu kwa kutumia mashine maalumu (dialysis) au kupandikiza nyingine.
Ingawa matibabu ya figo yameimarika, bado mtu anaweza kudumu na
tatizo hilo kwa miaka 20 hadi 30. Asilimia 20 ya watu wanaotibiwa kwa dialysis
huwa wamechelewa kugundua matatizo hayo kwa muda mrefu.
Baadhi ya matatizo ya figo yanaweza kutibika hadi kurejea kwenye
hali yake ya kawaida. Kwa bahati mbaya magonjwa ya figo huendelea na figo
zisiwezekane kabisa kurudia kwenye hali yake ya kawaida.
Jinsi figo zinavyofanya kazi
Figo zina jukumu kubwa katika mwili, siyo tu kuchuja uchafu
kwenye damu ili kuepukana nao, pia kuratibu madini yaliyomo ndani ya damu,
shinikizo la damu na kuchochea uzalishaji wa chembechembe nyekundu za damu.
Figo huwa zinakaa karibu na tumbo mbele ya ukuta wa mgongo na
ziko mbili kila upande wa uti wa mgongo. Zinapata damu kutoka kwenye mishipa ya
ateri moja kwa moja kutoka kwenye mshipa mkuu wa aota na kuirudisha damu hiyo
moja kwa moja kwa mishipa ya veini kwenda kwenye vena cava.
Figo zina uwezo wa kufuatilia kiwango cha umaji maji wa damu,
kuongezeka kwa madini kama vile sodiamu na potasiamu na tindikali kwa mwili
mzima. Huchuja uchafu wa vyakula vilivyosharabiwa mwilini. Uchafu mkubwa
unaochujwa mwilini ni pamoja na urea ya nitrojeni (blood urea
nitrogen-BUN) na creatinine (Cr).
Damu inaposhuka kwenye figo, vichocheo vyake huamua kiasi cha
maji kiende kuwa mkojo kulingana na uwingi wa madini yaliyomo ndani ya damu.
Kwa mfano, kama mtu anaharisha au ameishiwa na maji kutokana na ugonjwa mwingine,
figo huzuia maji yaliyopo yasiende kuwa mkojo na hapo mkojo huwa wa njano.
Lakini kama maji yako mengi mwilini, mkojo huwa na maji na
msafi. Kazi hiyo hufanywa na homoni inayoitwa renin ambayo huzalishwa na figo
ikiwa ni sehemu ya uratibu wa shinikizo la damu na hali ya mwili.
Figo pia huzalisha homoni ya ‘erythropoietin’ ambayo huchochea
uti wa mgongo kuzalisha chembechembe nyekundu za damu. Kuna seli maalumu katika
figo ambazo huratibu kiwango cha hewa ya oxygen ndani ya damu. Kama kiwango
hicho kitashuka ‘erythropoietin’ huongezeka na kuchochea uzalishaji wa chembe
nyekundu za damu.
Baada ya figo kuchuja uchafu, mkojo huzalishwa na kupelekwa
kwenye kibofu kupitia mrija wa ureta. Hutunzwa hapo ukisubiri mtu, mnyama
akojoe.