WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeagiza kutoka nje ya nchi tani 70,000 za sukari ambapo kati ya hizo, tani 11,957 zimeshawasili nchini na zitaanza kusambazwa kesho (Jumatano).
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumanne, Mei 10, 2016) wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano uliofanyika nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Akitoa ufafanuzi wa sukari ambayo imekwishawasili nchini, Waziri Mkuu alisema tani 2,000 zitapelekwa mikoa ya Kaskazini, tani 3,000 (mikoa ya Kanda ya Ziwa), tani 2,000 (mikoa ya Kusini), tani 2,000 (Nyanda za Juu Kusini) na tani 2,000 (mikoa ya Kanda ya Kati).
“Tani nyingine 24,000 za sukari zitawasili Ijumaa hii na hadi zitoke bandarini itakuwa kama Jumapili kwa hiyo zinaweza kusambazwa kuanzia Jumatatu. Tani nyingine 20,000 zitawasili baadaye, ama mwishoni mwa mwezi huu au mapema mwezi Juni,” alisema Waziri Mkuu.
Amesema anawataka Watanzania wasihofu kuhusu uhaba wa sukari uliojitokeza hivi karibuni kwani umesababishwa na watu wachache. “Mheshimiwa Rais ameagiza watu waliohodhi bidhaa hii wakamatwe na sukari isambazwe. Lakini pia tunaagiza kwa muda mfupi kwa sababu viwanda vyetu vinatarajia kuanza uzalishaji ifikapo Julai,” alisema.
Amewataka wasambazaji wa sukari waziuze kwa wafanyabishara wadogo ili wao wawawuzie wananchi kwa bei elekezi ya sh. 1,800. Pia amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanasimamia zoezi la ukaguzi ili kubaini zaidi wale waliohodhi bidhaa hiyo.
Akifafanua kuhusu mkakati wa Serikali kuongeza uzalishaji wa sukari nchini, Waziri Mkuu amesema nia ya Serikali ni kuhakikisha tatizo la uhaba wa sukari nchini linakwisha ifikapo 2019. “Wananchi wasiogope, Serikali imechukua hatua kwa udhibiti mzuri ili tusije kuporomosha soko letu la ndani,” alisema.
“Tunao mkakati wa kuboresha viwanda vya ndani, wenye viwanda wenyewe au kwa ubia na wawekezaji kutoka nje, wanaweza kufungua mashamba kwenye maeneo matatu tuliyotenga kwa ajili hiyo,” alisema.
“Serikali imetenga maeneo matatu yanayofaa kwa kilimo cha miwa huko Bagamoyo, Ngerengere na Kigoma. Huko wanaweza kulima na kujenga viwanda vya sukari na uzalishaji ukawa unapanda mwaka kwa mwaka hadi tutakapoweza kuimaliza hii gap iliyopo,” alisema.