Mwimbaji Jamala kutoka Ukraine aliipatia nchi yake ushindi wa pili katika shindano la wimbo barani Ulaya maarufu kama Eurovision usiku wa kuamkia leo Jumapili(15.05.2016).
Wimbo ulioshinda unaozungumzia madhila ya mizozo, na wimbo wa mwimbaji huyo uliishinda kidogo tu Australia na Urusi.
Wimbo huo unaoonesha masikitiko, uliopewa jina la 1944, umesababisha mabishano makali kutokana na kukumbusha mwaka ambao dikteta wa iliyokuwa Umoja wa Kisovieti Josef Stalin alipoamuru kuondolewa kwa watu wa kabila la wachache la watarta kutoka jimbo la Crimea kwenda Asia ya kati.
"Iwapo unaimba juu ya ukweli, inaweza kuwagusa hasa watu," amewaambia waandishi habari baada ya ushindi wake. Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 32, ambae jina lake halisi ni Susana jamaladynova na ni kutoka kabila la Tartar binafsi , amesema alihamasika kuutunga wimbo huo kutokana na madhila ya mustakabali uliomkumba nyanya yake mkuu.
Wimbo huo unaanza kwa maneno "Wakati wageni wakija .... wanakuja katika nyumba yako, wanawauwa wote na kusema, hatuna hatia hatuna hatia." Jamala amesema angependa kwamba "mambo yote hayo mabaya hayangetokea na kwamba wimbo huu haungekuwapo."
Anataka amani na mapenzi
Urusi ililichukua eneo la rasi ya Crimea mwaka 2014 na imewaunga mkono wapiganaji wanaotaka kujitenga wanaoiunga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine.
Mara baada ya kutangazwa mshindi akipata alama 534, Jamala alisema anataka "amani na mapenzi kwa kila mtu."
Ushindi huo , ambao umekuja usiku wa manane mjini Stockholm , ni wa pili kwa Ukraine, ambayo ilishinda mara ya kwanza tuzo hiyo mwaka 2004.
"Umetengeneza wakati murua kwa Ulaya leo. Kilikuwa kitu ambacho kinaendelea kwa muda mrefu," amesema Jon Ola sand wa Umoja wa vyombo vya utangazaji barani Ulaya (EBU), chombo ambacho kinaendesha mashindano hayo.
Mwimbaji wa Urusi
Kama mshindi, Ukraine itakuwa mwenyeji wa mashindano mengine mwaka ujao. Sand, msimamizi mkuu wa EBU katika Eurovision, aligusia suala la mzozo wa Ukraine, akisema ni muhimu "kuhakikisha kwamba kila mjumbe, kila mwandishi habari, kila shabiki ambae atataka kusafiri kwenda Ukraine aweze kusafiri kwa usalama, na kukaa huko akiwa salama." Australia, ikiwakilishwa na mwimbaji mwanamke Dami Im, ilipata alama 511.
Uimbaji wa Dami Im ulimpa kura miongoni mwa majaji 42 wa kitaifa.
Sergey Lazarev wa Urusi , ambaye alionekana kuwa mmoja kati ya waimbaji waliopewa nafasi ya kushinda , alimaliza akiwa watatu akipata alama 491, licha ya kushinda kura za watazamaji.
Alitumia picha za kupendeza zilizowekwa kwa ufundi wa hali ya juu jukwaani katika wimbo wake You Are The Only One.
Tamasha hilo la muziki katika ukumbi wa Globe mjini Stockholm lilifunguliwa kwa washiriki wote 26 kuingia jukwaani wakati bendera zao za taifa zikiwekwa katika ukuta kwa picha.
EBU imesema kujumuishwa kwa Australia katika shindano hilo kwa mara ya pili ni kutambua kuwapo kwa mashabiki wengi wa shindano hilo nchini humo na historia ya miaka 30 ya kulitangaza shindano hilo, ambalo ni tukio kubwa la televisheni katika bara la Ulaya.