WABUNGE wa kambi ya upinzani wameibuka na mbinu mpya kwa kuamua kujirekodi wenyewe sauti kwa kutumia simu za mikononi, wakati wakitoa michango yao bungeni kisha kutuma michango hiyo kwenye mitandao ya kijamii kama WhatsApp na redio zilizo majimboni mwao.
Hatua hiyo imetokana na Bunge kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya televisheni na redio, pamoja na kuzuia waandishi wa habari wa televisheni kurekodi shunguli zinazoendelea kwenye chombo hicho cha kutunga sheria.
Baada ya Bunge kukataza matangazo hayo ya moja kwa moja, kipindi maalumu cha saa moja kilianza kurushwa kwenye Televisheniya Taifa (TBC), ambayo huonyesha baadhi ya michango ya wabunge huku wale wa upinzani wakidai michango yao imekuwa haionyeshwi vya kutosha kwenye kipindi hicho.
Pia tangu kuanza kwa bunge hili la bajeti, ofisi ya Bunge imekuwa ikirekodi mijadala inayoendelea kisha kuwapa video waandishi wa habari wa televisheni.
Imekuwa ikidaiwa baadhi ya michango ya upinzani ama imekuwa haitolewi na ofisi hiyo kwenye video hizo au kutopelekwa kwa umma.
Akizungumzia suala hilo, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alisema wameona ni vyema wajirekodi wenyewe kwa simu na kutuma taarifa zao kwenye mitandao ya kijamii na kwenye redio za majimboni mwao (community radio).
“Tunatuma kwenye makundi ya WhatsApp, nyingine tunatuma makao makuu ya chama na kuzisambaza," alisema Msigwa. "Kwa mfano mimi ile ya kwangu imerushwa kwenye redio zote za Iringa.
” Alisema wameanzisha mbinu hiyo baada ya kukatazwa kwa matangazo ya moja kwa moja huku kile wanachoongea bungeni kikiwa kinakatwa na watumishi wa Bunge wanaotoa video za mijadala ya muhimili huo kwa waandishi wa habari.
Alipoulizwa endapo jambo hilo linaruhusiwa kikanuni, Naibu Katibu wa Bunge, John Joel, alijibu kwa kifupi kwamba haliruhusiwi.
Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, alipotafutwa ili kuzunguzia kwama mpango huo ni wa chama ama wabunge wenyewe, alisema jambo hilo siyo la chama na kwamba wanaosambaza sauti hizo siyo lazima wawe wabunge wao tu.
“Yawezeekana hata hao wabunge wa CCM wanazisambaza kuliko hata tunapozisambaza sisi, kwa sababu wabunge wetu wanaongea mambo mazuri ambayo wao hawawezi kuyazungumzia,” alisema Makene.
Mbinu hiyo mpya imeanza baada ya wabunge hao kuanza kuchangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na Utawala Bora na Menajimenti ya Utumishi wa umma.
Wabunge ambao hotuba zao zilianza kurekodiwa na kurushwa mitandaoni ni Godbless Lema, Mbunge wa Arusha mjini, Mchungaji Msingwa, Cecilia Paresso (Viti maalumu), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini) na Saed Kubena (Ubungo), wote wa Chadema.
Katika mchango wake, Msigwa pamoja na mambo mengine alisema Bunge limekuwa limekuwa likipelekeshwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, mpaka kufika hatua ya kupeleka Sh. bilioni sita kwa Rais John Magufuli bila ridhaa ya chombo kinachosimamia Bunge.
Naye Lema, pamoja na mambo mengine, alisema Dk Tulia amekuwa akijifanya ni Spika na kwamba alichukua hatuaya kupeleka fedha hizo bila Spika wa Bunge, Job Ndugai kujua, na kwamba kiongozi huyo wa muhimili huo alipata taarifa za fedha hizo kupelekwa kwa rais kwenye mtandao wa WhatsApp.