Watu wanaodhaniwa kuwa ni wakufurishaji wamevamia msikiti wa ‘Masjid Rahma’ mkoani Mwanza, Tanzania na kufanya mauaji.
Kwa mujibu wa mashuhuda mauaji hayo yalitokea jana usiku kwenye msikiti huo uliopo eneo la Ibanda Relini, kata ya Mkolani wilayani Nyamagana. Habari zaidi zinasema kuwa, kundi la watu wanaokadiriwa kama 15 na ambao walikuwa wamejifunika nyuso zao, waliwavamia Waislamu waliokuwa wakisali sala ya Isha ndani ya msikiti huo na kuanza kuwakatakata kwa mapanga. Miongoni mwa watu waliouawa katika hujuma hiyo ni pamoja na imamu wa msikiti huo, Ferouz Elias, Mbwana Rajab na Khamis Mponda ambaye ni dereva wa bodaboda. Aidha watu wengine walijeruhiwa katika tukio hilo. Mashuhuda wameeleza zaidi kuwa, wakati waumini hao walipokuwa wakiendelea na ibada ya Sala, ghafla kundi la watu hao waliingia msikitini hapo na kuanza kuhoji kwamba, ni kwanini walikuwa wanaswali ilhali wenzao wamekamatwa na kuendelea kushikiliwa na polisi, kauli ambayo iliendana na mashambulizi hayo. Habari zaidi zinasema kuwa, washambuliaji hao walikuwa na bunduki aina ya SMG pamoja na mabomu ya kutengeneza ambapo baada ya tukio hilo walirusha mabomu hayo lakini hayakuleta madhara yoyote.
Kufuatia hujuma hiyo, Shekh Hussein Ibrahim, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Wilaya ya Nyamagana mbali na kulaani kitendo hicho, amesema vitendo vya namna hiyo havikubaliki katika Dini ya Kiislamu na kwamba, Waislamu wote wanapaswa kulaani matukio ya namna hiyo. Inafaa kuashiria kuwa, kwa muda mrefu kumekuwepo ugomvi kati ya waumini wa msikiti wa Rahma ambao ni wa Waislamu wa Kisuni na wale wa Kiwahabi, ugomvi ambao ulipelekea hivi karibuni polisi ya Mwanza kuwatia mbaroni vinara wa Kiwahabi.