Mke
wa askari polisi wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki), Sajenti Ally Salum
(Kinyogori) aliyeuawa hivi karibuni, amekiri kuhusika kwenye mauaji hayo,
akidai ilitokana na mumewe kumuacha na kuoa mke mwingine.
- Alimuua kwa kumtuma mtu mwingine kutekeleza mauaji hayo kwa
sababu ya kuachwa na mumewe
Kamanda wa Polisi, Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa
mwanamke huyo anashikiliwa na polisi kwa mauaji hayo yaliyofanyika nyumbani kwa
Kinyogori, Mkuranga mkoani Pwani.
Wakati huo huo, Kamanda
Sirro amezungumzia pia mauaji ya Anathe Msuya yaliyofanyika hivi karibuni
Kigamboni na kusema polisi inaendelea kumtafuta msichana wa kazi za nyumbani
aliyetoroka siku moja kabla ya kifo cha mwanamke huyo.
Anayetuhumiwa kuua
mumewe
Akizungumza na waandishi
wa habari jana kuhusu matukio mbalimbali ya uhalifu yaliyojitokeza jijini Dar
es Salaam, Sirro alisema katika mahojiano ya awali mke wa Kinyogori amekiri
kuhusika.
Kwa mujibu wa kamanda,
mwanamke huyo ambaye hata hivyo hakutaja jina lake kwa sababu za kipelelezi,
aliamua kumtuma mtu kutekeleza mauaji hayo baada ya mumewe kumwacha na kuoa mke
mwingine.
“Ni jambo la kusikitisha
kuona mtu anatoa uhai wa mtu sababu ya kuachwa. Tunawasihi wananchi kuepuka
kujihusisha na matukio kama haya, eti sababu tu ya kuachwa wanawake wapo wengi
na wanaume wapo wengi unaweza kuachwa na ukaolewa na ukaoa kuliko kuondoa uhai
wa mtu,” alisisitiza Sirro.
Hata hivyo, Sirro
alisema wanaendelea kuwahoji watuhumiwa hao ili waweze kuwataja watu wengine
walioshirikiana nao kutekeleza tukio hilo baada ya kuonekana kuwepo kwa
wahusika wengine.
‘Hausigeli’ asakwa
Kuhusu mauaji ya Anathe
aliyechinjwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni, Kamanda Sirro alisema
wanaendelea na jitihada za kumtafuta msichana huyo ahojiwe kuhusu tukio hilo.
Aidha alisema mtu mmoja
anashikiliwa akituhumiwa kuhusika na tukio hilo huku polisi ikiwa imeandaa timu
ya upelelezi itakayoshughulikia tukio hilo kufanikisha kuwakamata wote
waliohusika na tukio hilo.
Sirro alisema msichana
huyo aliondoka siku moja kabla ya tukio hilo la mauaji hivyo kupatikana kwake,
kunaweza kusaidia polisi kujua kama kuondoka kwake kulikuwa salama au kuna kitu
kimejificha.
“Msichana huyu
tunaendelea kumsaka tujue kama aliondoka salama na kumhoji zaidi juu ya
kuondoka kwake siku moja tu, tukio linatokea nina imani tutafanikiwa kumpata na
wote waliohusika na kukomesha matukio haya,” alisema Sirro.
Mamia wajitokeza msibani
Vilio na simanzi jana
vilitawala wakati mamia ya wakazi wa Kibada Kigamboni na Salasala walipokuwa
wakiuaga mwili wa marehemu Anathe Msuya (30), aliyeuawa Mei 25 nyumbani kwake
kwa kuchinjwa na watu wasiojulikana.
Mwili ulichukuliwa jana
asubuhi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili na kupelekwa nyumbani kwake Kibada,
kwa ajili ya kuagwa na majirani zake kabla ya kusafirishwa kwenda kuzikwa
mkoani Arusha leo.
Akizungumza baada ya
mamia kumuaga nyumbani kwa marehemu, mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Nyakwale
Kibada, Said Pazi alisema kuwa wao kama majirani waliomba familia wapate fursa
ya kumuaga jirani yao ambaye tangu ahamie ana muda wa miezi sita.
“Baada ya kuambiwa msiba
upo Salasala tuliomba kama majirani na sisi tupatiwe fursa ya kuuaga mwili wa
ndugu yetu ambaye alihamia mwaka jana… kwa kweli msiba wake umetusikitisha
sana” alisema.
Akizungumzia tukio hilo
alisema kuwa mtoto wa marehemu huyo, Allan Kimario (4) aliwataarifu majirani
kuwa mama yake haamki na ndipo walipofika wakakuta ameuawa.
Mwenyekiti huyo alitoa pole na kusema atahakikisha wanaimarisha ulinzi
na kuhimiza wenye viwanja ambavyo havijajengwa, wavifanyie usafi ili kuondoa
vichaka ambavyo ni hatari kwa usalama