MKUU
wa Chuo cha Uhasibu (IAA) Njiro mkoani Arusha, Profesa Johannes Monyo
amehukumiwa kifungo cha nje kwa sharti la kutofanya kosa lolote ndani ya
mwaka mmoja.
Hukumu
hiyo ilitolewa Ijumaa iliyopita na Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya
Arusha, Devotha Msofe baada ya kujiridhisha kuwa Profesa Monyo alifanya
makosa ya kuajiri watumishi wanane wenye elimu ya darasa la saba bila
kufuata misingi na kanuni za utumishi wa umma.
Hakimu
Msofe alisema Profesa Monyo akiwa Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Njiro,
aliwaingiza watumishi wanane kwenye ajira ya kudumu bila ya kibali
kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi au Katibu Mkuu Utumishi.
Alisema
kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani kwa mashahidi 10 pamoja na
vielelezo vinane vilivyotolewa mahakamani hapo na upande wa mshtakiwa
kuwa na mashahidi wawili, mahakama hiyo imejiridhisha pasipo shaka kuwa
Profesa Monyo alifanya kosa hilo la kuajiri wafanyakazi hao wanane bila
kufuata taratibu za kisheria.
“Mahakama
imejiridhisha pasipo shaka kuwa ulifanya kosa hili la kuajiri
wafanyakazi wanane bila kufuata misingi na kanuni za utumishi wa umma
hivyo mahakama hii inakutia hatiani kwa kukupa kifungo cha nje kwa
sharti la kuutofanya kosa lolote katika kipindi cha mwaka mmoja,” alisema Hakimu Msofe.
Awali,
Mwanasheria kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),
Adam Kilongozi alidai kuwa Juni, 2010 Profesa Monyo anatuhumiwa kuwapa
ajira watumishi wanane ambao ni Pamela Maboko, Samson Mbarya, Mawazo
Ndaro, Juma Nyarutu, Lilian Ngowi, Godfrey Mollel, Musa Maiki na Salim
Shabani.
Kosa jingine ni Profesa Monyo kwa kutumia mamlaka yake vibaya, kuwaingiza watumishi hao wanane katika ajira, ilhali akijua elimu zao ni darasa la saba.
Hata hivyo, baada ya hukumu hiyo kutolewa, Profesa Monyo ameonesha
kusudio la kukata rufaa kupitia kwa wakili wake, Severine Lawena.
Baada
ya hukumu hiyo kutolewa, mwandishi alimhoji Mwanasheria wa Takukuru,
Kilongozi, kuhusu Sheria ya Utumishi wa Umma au Kanuni zake inasemaje
juu ya mtumishi anapohukumiwa akiwa bado yupo kazini, ambapo alisema
kama mtuhumiwa amehukumiwa na akaonesha nia ya kukata rufaa, basi hukumu
hiyo inaweza kufanya kazi au kutofanya kazi hadi hapo rufaa
itakaposikilizwa.
Alisisitiza
kuwa Takukuru wameshatuma nakala hiyo ya hukumu Tume ya Utumishi wa
Umma, mwajiri wa Profesa Monyo, ili mamlaka husika zilifanyie kazi suala
hilo lakini pia ni lazima mwajiri wake naye ajiridhishe na hukumu hiyo.